Breaking News

WATANZANIA WAHIMIZWA KUSAIDIA WATU WENYE MAHITAJI MAALUMU

WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kusaidia watu wenye mahitaji maalumu ili kuondoa dhana kwamba watu wa aina hiyo wametengwa na jamii na hapaswi kusaidia kwa namna yoyote.

 Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi Stella Manyanya, Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Rukwa, Wallace Kiama  ametoa wito huo jioni ya leo wakati wa harambee ya kuchangisha fedha ya kununua gari kwa ajili ya kituo cha watoto yatima wa kituo cha Katandala St Martin de Pores,kilichopo mjini hapa, ambayo iliandaliwa na Chama cha Maendeleo ya Wanawake Sumbawanga (SWAA).

Alisema kuwa jamii ya watanzania imekuwa haina utaratibu wa kuwatembelea na kuwasaidia watu wenye mahitaji mbalimbali kama yatima hivyo watu hao kuona kama watengwa na sio sehemu ya jamii yetu kitu ambacho kinawafanya baadhi yao kukata tamaa ya maisha."watu wenye mahitaji mbalimbali ni wengi kuna watoto wa mitaani, yatima, wazee na wagonjwa ambao wapo hospitalini na majumbani, sasa tujenge utamaduni wa muda tunaopata kuwatembelea ikibidi kutoa chochote tulichonacho ili wasijione kuwa wametengwa na wengine wasikate tamaa kwa sababu ya maradhi yanayowasumbua" alisema Manyanya

Aliongeza kuwa mathalani baadhi ya wagonjwa wamepoteza maisha kwa kukataa tamaa kwa kudhani kwamba maradhi yanayowasumbua hawezi kupata tiba hivyo wagonjwa wa aina hiyo wanapaswa kutembelewa na kufarijiwa ili waondokane na dhana hiyo.

Manyanya alitoa wito kwa wafanyabiashara na watu wenye kujiweza kiuchumi kutumia sehemu ya faida wanayopata kurejesha kwa jamii kwa kusaidia watu wenye mahitaji mbalimbali kama makundi ya yatima na wagonjwa badala ya kufanyia starehe na hanasa zisizo za msingi.




Awali, akisoma risala ya Chama hicho Makamu Mwenyekiti wa SWAA, Hamida Seif alisema lengo la kufanya harambee hiyo ni kukusanya fedha kiasi cha Sh milioni 20 kwa ajili ya kununua gari aina ya Noah ili liweze kuwasaidia watoto hao kwa matumizi mbalimbali yakiwemo ya kuwapeleka hospitali pindi wanapougua.

Alisema kuwa hivi sasa kituo hicho hakina usafiri hali ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu na kero kubwa kwao hasa watoto wanapougua kwani hulazimika kutafuta magari ya kukodi ambapo nyakati za usiku gharama huwa kubwa sana.
"tulitembelea kituo cha watoto yatima Katandala tukaona kuna changamoto ya ukosefu wa usafiri......sasa kwa kupitia Swaa tukaona kuna uwezekano wa kufanya harambee ili kuita wadau mbalimbali watusaidie kukusanya fedha za kununua gari hilo" alisema Seif.

Aidha, Mwenyekiti Swaa Grentina Kalinga alisema kuwa pamoja na harambee hiyo kutofana kutokana na watu wachache kujitokeza tofauti na makadirio yao hivyo kufanya kupatikana kiasi cha Sh milioni 4 bado watawasiliana wadau waliowaalika ili waweze kuwachangia hali ambayo itasaidia kufanikisha kufikia lengo lao kununua gari kwa ajili ya kituo hicho.
Kituo cha St Martin de Pores,  kina watoto yatima 40 ambapo kina uwezo wa kupokea watoto hadi 100 ambapo wengi wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho ni wale waliofiwa na wazazi wao hivyo kukosa watu wa kuwalea.

No comments