Breaking News

SHEHENA YA MAGOGO YA MAMILIONI YANASWA RUKWA

SHEHENA kubwa ya magogo yenye thamani ya zaidi Sh milioni 80 imekamatwa ikiwa imevunwa kinyume na utaratibu katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa.

Afisa maliasili mkoa wa Rukwa, Nicholaus Mchome alisema jana wakati akizungumza na mwandishi wa blog ya Pembezonikabisa ambapo alidia kuwa shehena hiyo imekatwa kufuatia operesheni iliyofanywa na kikosi cha maliasili kinachodhibiti uvunaji haramu wa misitu.
Alisema kuwa magogo hayo yatokanayo na misitu yanakadiriwa kufikia zaidi 1500 ambapo yamevunwa bila kufuata utaratibu wa kupatiwa vibali vinavyowaruhusu kufanya zoezi hilo.
Mchome alisema kuwa kukamatwa kwa magogo hayo ni kufuatia taarifa zilizopatikana kwamba wapo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakivamia misitu na kuvuna misitu hiyo bila kufuata sheria.
"Tunaishukuru serikali imesaidia nyezo kwa haraka kuwezesha kukamata kwa magogo hayo, maana wenzetu wanatumia udhaifu wetu wa kukosa vitendea kazi kwa hiyo wanafanya uvamizi kuendesha uvunaji haramu" alisema

Aliongeza kuwa athari zitokanazo na uvunaji wa aina hiyo ni pamoja na kulikosesha taifa mapato, kuharibu mazingira, pia kuvuna misitu isiyotakiwa ambapo kama wangefuata utaratibu wangeelezwa aina ya miti inayoruhusiwa kuvuna ili kuepuka kutokea kwa athari za kimazingira.
Aidha, uchunguzi uliofanywa umebaini kwamba zoezi la uvunaji haramu mazao hayo ya misitu unafanywa na mmoja wa wafanyabiashara kutoka nchi jirani akishirikiana na baadhi ya wananchi wasio waaminifu.
Inadaiwa kuwa baada ya kuvuna magogo hayo, uyapeleka nchi jirani ya Zambia kisha kuyangiza nchini kupitia mpaka Tunduma na kulipiwa kama mzigo kutoka nje ya nchi kisha kusafirishwa kuelekea nchini china ambako ndiko kuna soko zuri la magogo hayo yanayotumika kwa kutengenezea samani za ndani.
Mchome alipoulizwa juu ya hilo, alikiri kusikia taarifa hizo, lakini akaeleza kuwa uchunguzi unaendelea kufanyika ili kujua ukweli wa hilo na hatua za kisheria zitafuata mkondo iwapo watu hao watabainika.Aidha, Ripoti ya Kitengo cha Udhibiti na Utafiti katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iliyotolewa mwaka 2014 inaeleza kuwa upungufu mkubwa wa watumishi na vitendea kazi katika sekta ya misitu umeathiri usimamizi endelevu wa rasilimali ya misitu nchini huku asilimia 82 ya watu waliohojiwa walisema uvunaji haramu wa mazao ya misitu unachochea biashara hiyo.

Vilevile, imebainika kuwa asilimia 71.9 ya misitu inavunwa bila vibali, huku maeneo yasiyoruhusiwa ni asilimia 70.3, uvunaji wa miti isiyokomaa asilimia 73.4 na miti inayozidi kiasi kilichopangwa kuvunwa asilimia 67.2.
Mikoa ya Kigoma, Pwani, Ruvuma na Tabora imetajwa kukithiri wa uvunaji haramu wa misitu ya asili. Asilimia 73.7 ya mazao ya misitu yamesafirishwa kwa njia za panya na matumizi ya kibali kimoja cha kusafirishia zaidi ya mara moja kwa asilimia 64.4.



No comments