M’kiti atupwa jela miezi sita kwa ‘kumtwanga’ daktari
Na Mwandishi wetu, Mpanda.
Mahakama
ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, imemuhukumu kifungo cha miezi sita jela
Mwenyekiti wa Kijiji cha Simbwesa, Mabula Gilede (30), kwa kosa la kumpiga na
kumjeruhi daktari wa zahanati ya kijiji hicho, Dk Lazaro Michael.
Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Odila Amwol baada ya
kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na kumtia hatiani mshtakiwa
huyo.
Awali
Mwendesha Mashtaka, Kulwa Kusekwa alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo
Agosti 19, mwaka jana katika Zahanati ya Simbwesa baada ya kumtuhumu daktari
huyo kuwa alikuwa akitoa matibabu kwa wagonjwa kwa upendeleo.
Alidai
siku ya tukio, mshtakiwa huyo alikwenda kwenye zahanati hiyo na kumshambulia
kwa kumpiga kwa mateke na ngumi mganga huyo kwa madai anawatibu wafuasi wa CCM
na kuwaacha wa Chadema.
Kusekwa
aliendeela kudai kabla ya tukio hilo, mshtakiwa huyo alidai kuwa daktari huyo
alikataa kumtibu mtoto wa rafiki yake aitwaye Milembe Machime ambaye ni mfuasi
wa Chadema.
Hata
hivyo, katika utetezi wake, mshtakiwa huyo aliyekuwa akitetewa na Wakili
Patrick Mwakyusa alidai kuwa hakumpiga daktari huyo kama inavyodaiwa.
Alidai
daktari huyo ndiye aliyempiga hadi kumuangusha chini kwa sababu alimuuliza
kwanini alikataa kumtibu mtoto wa rafiki yake huyo.
Hakimu
Odira kabla ya kusoma hukumu, aliiambia Mahakama kuwa kutokana na mwenendo
mzima wa kesi hiyo na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa
mashtaka, Mahakama imemwona mshtakiwa ana hatia.
Katika
utetezi uliotolewa na mwanasheria wa Gilede, Patrick Mwakyusa, aliiomba
Mahakama impunguzie adhabu kwani mshtakiwa huyo ana wake watatu na watoto, pia
mama yake mzazi anamtegemea.
No comments