Breaking News

Acheni kupeleka wagonjwa wa kipindupindu kwa waganga wa kienyeji.

Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Dk. Halfan Haule akiwaelimisha wananchi wa kata ya Mtowisa wilayani Sumbawanga vijijini kuhusu matumizi ya kanuni za afya ili kujiepusha na ugonjwa wa kipindupindu ambao umeua watu nane hadi sasa na wengine 157 Kulazwa katika vituo vinavyotoa huduma ya afya.

Na Mwandishi wetu. 

Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa,  Dk. Halfan Haule amewataka wakazi wa bonde ziwa Rukwa, kuacha tabia ya kuwapeleka wagonjwa wa kipindupindu kwa waganga wa kienyeji badala yake wawapeleke vituo vinavyotoa huduma za afya ili kupata tiba za kitaalamu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Mtowisa wilayani Sumbawanga mkoani humo.

Alisema tabia ya baadhi ya wananchi kuendekeza imani za kushirikina na kuwapeleka wagonjwa wa kipindupindu kwa waganga wa kienyeji kunahatarisha maisha ya wagonjwa hao na wakati mwingine kusababisha vifo.

Alisema jamii ya watu wa bonde la ziwa Rukwa ambako ugonjwa huo umeenea ipo haja sasa kubadilika na kuachana na tabia hiyo, hivyo wawapeleke wagonjwa wao katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ili wapate tiba sahihi ambazo zitaokoa maisha yao. 

Dk. Haule alipiga marufuku tabia ya kaya moja kutumia choo kimoja badala yake alitaka kila kaya kuwa na choo chake na kaya isiyokuwa na choo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dk. Halfan Haule akigawa dawa za kutibu maji kwa wakazi wa kijiji cha Muze jana wakati wa ziara yake ya kuelimisha wananchi kuhusu maradhi ya kipindupindu.

Awali,mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Fani Mussa alisema kuwa tangu ugonjwa wa kipindupindu uingie katika halmashauri hiyo siku 53 zilizopita jumla ya wagonjwa 165 wameugua kulazwa katika vituo vinavyotoa huduma ya afya  ambapo nane kati yao wamefariki dunia.

Alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa pamoja na kuchukuliwa kwa sampuli 15 ambazo zilithibitisha kuwa na ugonjwa huo hivyo kusambaza dawa na vifaa tiba katika kambi mbalimbali zilizofunguliwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hao.

Alisema kuwa elimu ya afya inayolenga kuwahamasisha wananchi kuzingatia kanuni za afya, ikiwa pamoja na kuchemsha maji kabla kunywa na kunawa mikono baada kutoka chooni imetolewa kwa wakazi wa bonde la ziwa Rukwa ambalo vijiji vyake vingi vimeathirika na malazi hayo. 

Dk. Mussa alisema watu 14 kati ya 58 Waliokamatwa kwa kukiuka kanuni za afya ikiwa pamoja na kaya zao kutokuwa na vyoo wamehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela.

Mwisho

No comments