Breaking News

Msakila Day yaadhimishwa kwa stahili ya aina yake!.

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Msakila iliyopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, wakifanya usafi katika viunga vya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa.

Mussa Mwangoka, Rukwa

Wakazi wa mkoa wa Rukwa wamehamasishwa kujenga utamaduni wa kujitolea damu ili kuweza kusaidia wagonjwa mbalimbali wenye mahitaji hayo wakiwemo wakina mama wajawazito ambao upoteza damu nyingi wakati wa kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Rukwa, Dk. John Lawi alisema hayo leo wakati akitoa shukrani zake kwa uongozi wa kanisa katoliki baada ya kuhamasisha waumini wake kujitolea damu na kufanya usafi katika hospitali hiyo.

"Tunashukuru sana kwani tumepata chupa chupa 42 za damu ambazo zitasaidia kwa kiwango kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa wanapungukiwa na damu lakini pia wajawazito ambao hufika na kujifungua kwa njia ya upasuaji wengi wao upoteza damu nyingi na wakati mwingine kuhitaji kuongezewa" alisema Dk. Lawi

Aliongeza kwamba mahitaji ya damu katika hospitali hiyo ni 120 kwa mwezi hivyo ni wajibu wa jamii kujitokeza na kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa na hata majeruhi wa ajali wanaofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu.

Awali, Padri wa Kanisa Katoliki Christopher Mayemba alisema vijana wamejitolea kutoa damu na kufanya usafi hospitalini hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 24 ya kifo cha askofu wa kwanza wa jimbo katoliki la Sumbwanga, Askofu Karolo Msakila.

Alisema vijana hao waliona njia sahihi ya kumuenzi askofu huyo ni kujitolea damu ili kusaidia wagonjwa na kufanya usafi katika vuinga vya hospitali hiyo, kisha kufanya maandamano ya kuelekea kanisani kwa ajili ya ibada maalumu ya kumuombea marehemu askofu msakila.

Watawa na waumini wa Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga wanamkumbuka Askofu Msakila kwa kauli mbiu yake Tunda la roho ni upendo ambapo katika kipindi cha uhai wake alimudu kuunganisha vema tabia yake na kauli mbiu yake akiongozwa na neno la Mungu maana "Mungu hakutaka roho ya woga, bali nguvu na upendo na moyo kiasi"

Alifariki dunia feb 23 mwaka 1994 mjini Sumbawanga.

No comments