Wanaopata mimba katika umri mdogo wadhibitiwe, asema Padri
Na Walter Mguluchuma, Katavi.
Kasisi wa Kanisa Katoliki jimbo la Mpanda mkoani Katavi, Padri Leonard Kasimila ameshauri kwamba wasichana wanaopewa wanaopewa ujauzito wakiwa katika umri mdogo waanze kuchukuliwa hatua wao na wanaume zao ili kusaidia kupunguza tatizo la mimba za utotoni zilizokithiri mkoani humo.
Alisema katika utafiti wake mdogo amebaini kwamba tatizo la mimba za utotoni kwa asilimia 80 linasababishwa na wanaume na vijana wa kiume huku asilimia 20 likisababishwa na wasichana wenyewe kwa kuendekeza tamaa za kimwili.
Alisema ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo, ipo haja sasa ukaanzishwa utaratibu wa kuwakamata na kuwafungulia mashitaka watoto wa kike wanaopewa mimba huku pia wanaume waliohusika nao wakikamatwa na kuchukulia hatua stahiki.
Kasisi huyo alisema kitendo cha kutowachukulia hatua wasichana wanaopata ujauzito katika umri mdogo kunawafanya waone kitendo wanachofanya ni sahihi.
Hivi karibuni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliutaja Mkoa wa Katavi kuwa ndiyo unaoongoza nchini kwa kuwa na tatizo la mimba za utotoni, ambako tatizo hilo lipo kwa takribani asilimia 45.
Aidha, imetaja mikoa mingine inayofuatia kwa tatizo hilo, kulingana na asilimia kuwa ni pamoja na Mkoa wa Tabora (43), Dodoma (39), Mara (37) na Shinyanga (34). Kitaifa tatizo hilo lipo kwa asilimia 27.
No comments